Baba yake Nabii Yunus (alaihis salaam) alikuwa mtu mchamungu akiitwa Mattaa. Yeye na mkewe, kwa muda mrefu, walitamani kwamba Allah Ta’ala Awajaalie mtoto wa kiume na amweke kuwa Nabii wa Bani Israa’il.
Miaka mingi ilipita, huku wakiendelea kuomba dua, mpaka hatimaye, waliamua kwenda kwenye chemchemi iliyobarikiwa ya Nabii Ayyoob (alaihis salaam) na kuoga humo na akapewa shifaa kamili na Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah)
Wote wawili walikwenda kwenye chemchemi na kuoga maji yake. Baada ya hapo,
walijishughulisha na Swalah na wakamuomba Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah) awajaalie mtoto aliyebarikiwa ambaye atakuwa Nabii wa Bani Israa’il.
Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’alah) Akaikubali dua yao na mke wa Mattaa baada ya hapo akashika mimba ya Nabii Yunus.
Baada ya miezi minne ya ujauzito, wakati mtoto alikuwa bado tumboni, Mattaa alifariki dunia na kuiacha dunia hii.
Ingawa Mattaa hakuishi kuona matunda ya dua yake yakitimia, aliacha mwana mchamungu kama urithi wake ambao utaendelea kumpatia thawabu kubwa huko Akhera.
Uwekezaji Wa Akhera
Kutokana na tukio hili, tunaelewa kuwa urithi mkubwa zaidi ni urithi wa kizazi cha watu wema. Urithi huu ni kwamba hautamfaidisha mtu katika dunia hii tu, lakini faida yake itaendelea hadi Akhera.
Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) amesema: “Mtu anapofariki, vitendo vyake vyote hukatika isipokuwa kwa vitendo vitatu; Sadaqat-ul jaariyah (matendo yake mema ambayo thawabu zake zinaendelea baada ya kufariki kwake), elimu yake ambayo watu wananufaika nayo (baada ya kufariki kwake) na mtoto mchamungu anayemuombea dua.”
Wasiwasi na Dua ya Manabii (alaihimus salaam) kwa Vizazi vyao
Mtu anapochunguza maisha ya manabii (alaihimus salaam), Maswahaba (radhiyallahu anhum) na wachamungu wa zamani, atakuta kwamba waliomba dua maalum kwa ajili ya watoto wachamungu ambao watakuwa urithi kwao baada ya kufariki kwao.
Vile vile, walikuwa na wasiwasi juu ya maendeleo ya deeni cha kizazi chao katika maisha yao yote. Hivyo, Quraan Majeed inataja dua maalum ya Ibrahim na Zakariya (alaihimas salaam) kupata watoto wachamungu.
Vile vile, wakati Ya’qub (alaihis salaam) alipokuwa amelala kwenye kitanda chake cha mauti, aliwausia watoto wake kubaki imara katika Dini baada ya kufariki kwake. Wasiwasi wake mkubwa, hata alipokaribia mwisho wake, ulikuwa kwa ajili ya usalama wa deeni ya kizazi chake baada yake.
Wasiwasi wa Maswahaabah (radhiyallahu anhum) kwa Watoto zao
Baada ya Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) kuhijiria Madinah Munawwarah, Ummu Sulaim (radhiyallahu anha) alimleta mtoto wake Anas (Radhiyallahu anhu) kwake na akamwomba amkubali mtoto wake kuwa msaidizi wake.
Anas (Radhiyallahu anhu) alikuwa na umri wa takriban miaka kumi wakati huo. Alikaa katika utumishi uliobarikiwa wa Mtume (Sallallahu alaihi wasallam) kwa muda wa miaka kumi hadi alipofariki Rasulullah (sallallahu alaihi wasallam).
Bila shaka, ilikuwa ni wasiwasi wa dini na malezi ya mtoto wake uliomsukuma kumpeleka kwa Rasulullah (Sallallahu alaihi wasallam) na kumweka wakfu kwa utumishi wake.
Vile vile, Abbaas (radhiyallahu anhu) alimuelekeza mtoto wake mdogo, Abdullah bin Abbaas (radhiyallahu anhuma), kulala usiku pamoja na Mtume (sallallahu alaihi wasallam) kwenye nyumba ya shangazi yake, Maimoonah (radhiyallahu anha), ili kuswali Tahajjud yake na kunufaika na malezi yake uliobarikiwa.
Abdullah bin Abbaas (radhiyallahu anhuma) alikuwa takriban kumi na mbili au umri wa miaka kumi na tatu wakati huo.
Ni tamaa ya kila mzazi kwamba mtoto wake awe salama baada ya yeye kufa. Kwa hivyo, hatua zinazohitajika zinachukuliwa kuhifadhi na kulinda uwezo wa kifedha kwa mtoto.
Lakini, wasiwasi mkubwa wa mzazi unapaswa kuwa usalama wa dini wa mtoto, kwani hii ndiyo kitu pekee kitakachomhifadhi kushikamana na Allah Ta‘ala na kumpatia mafanikio katika dunia hii na ijayo.