Anas (radhiya allaahu ‘anhu) anasimulia kwamba katika tukio moja, Maswahabah (Radhiya Allaahu anhum) walikuwa wamekaa kwenye kundi lililobarikiwa la Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) aliposema: “Baada ya dakika chache atatokea mtu katika watu wa Jannah mbele yenu.” Hapo hapo, Sa’d (radhiyallahu anhu) alitokea, akiwa amebeba viatu vyake kwa mkono wake wa kushoto, huku ndevu zake zikitiririka na maji ya udhu.
Siku ya pili na ya tatu, Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) alitoa tangazo hilo hilo, na katika siku zote mbili, mtu aliyeingia alikuwa Sa’d (radhiya allaahu anhu).
Abdullah bin Amr bin Aas (radhiya allaahu anhuma) alitaka kutumia muda fulani kukaa pamoja na Sa’d (radhiya allaahu anhu) ili aweze kutazama tabia na matendo yake, na hivyo kugundua kitendo maalum alichokuwa nacho hadi Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) kamtolea bashara za Jannah.
Kwa hiyo, siku ya tatu baada ya Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) kutoka Abdullah bin Amr (radhiya allaahu anhuma) alisimama na kumfuata Sa’d (radhiyallahu anhu) ili kuzungumza naye. Alipokutana naye, Abdullah bin Amr (radhiya allaahu anhuma) akamwambia: “Nilikuwa na ugomvi na baba yangu, kwa hiyo niliapa kwamba sitarudi nyumbani kwa muda wa siku tatu. Je unaweza kunipa mahali pa kukaa nyumbani kwako hadi siku tatu zipite?”
Sa’d (radhiya allaahu anhu) alikubali na Abdullah bin Amr (radhiya allaahu anhuma) akaanza kukaa naye. Hata hivyo, pamoja na kumtazama katika zile siku tatu, Abdullah bin Amr (radhiyallahu anhuma) hakuona kitendo chochote ambacho alikiona kuwa ni cha ajabu. Kwa hakika, hakumuona Sa’d (radhiyallahu anhu) akiamka kuswali Tahajjud. Aliamka tu wakati wa alFajr. Lakini aliona kwamba wakati macho ya Sa’d (radhiya allaahu ‘anhu) yanapofunguka usiku na alikuwa akigeuka kutoka upande mmoja hadi mwingine kitandani, alikuwa akisoma dhikr kabla kulala.
Hata hivyo, sifa kuu ambayo Abdullah bin Amr (radhiyallahu anhuma) aliiona kwa Sa’d (radhiya allaahu anhu) ni kwamba alizungumza tu mema (kuhusu watu na hakuwahi kusema lolote baya kuhusu mtu yoyote).
Hatimaye, zilipotimia siku tatu, na Abdullah bin Amr (radhiya allaahu anhuma) hakuona jambo lolote lisilo la kawaida katika maisha ya Sa’d (radhiya allaahu anhu) ambalo aliweza kumnasibisha bashara za Jannah, aliamua kumwendea Sa’d (radhiyallahu ‘anhu) na kufichua sababu hasa ya kutaka kukaa naye kwa siku tatu.
Hivyo, alimwendea Sa’d (radhiya allaahu ‘anhu) na kusema, “Ewe mja wa Mwenyezi Mungu! Kwa kweli, sikuwa na iktilafu wala ugomvi au sikukataa kuongea na baba yangu.
Lakini sababu ya mimi kutaka kukaa na wewe ni kwamba kwa muda wa siku tatu mfululizo, Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) alitoa tangazo lifuatalo, “Mtu wa Jannah anakaribia kujitokeza kwenye mkusanyiko”, na katika zote siku tatu, wewe ulikuwa mtu aliyejitokeza. Ilikuwa ni kwa sababu hii kwamba nilitamani kukaa na wewe ili niweze kutazama tabia na mwenendo wako na kuiga sifa zako nzuri. Hata hivyo, (kwa kutazama matendo yako,) sikukuona unafanya vitendo vingi vya nafl, basi niambie kitendo maalum gani unachofanya kwa ajili yake ambacho umepata bashara njema za Jannah kutoka kwa Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam)? ”
Sa’d (radhiya allaahu ‘anhu) akajibu, “Vitendo pekee ambavyo ninavifanya ni vitendo ambavyo umeviona (yaani hakuna kingine katika maisha yangu ninachofanya isipokuwa yale uliyoyaona).” Aliposikia hivyo, Abdullah bin Amr (radhiya allaahu anhuma) aligeuka na kuondoka zake. Hata hivyo, alipokuwa anaondoka, Sa’d (radhiya allaahu anhu) alimwita tena na kumwambia, “Vitendo ninavyofanya ni vitendo ambavyo umeviona, lakini, kitendo kingine (ambayo inaweza kuwa sababu ya mimi kupokea bashara njema za Jannah) ni kwamba mimi sina chuki moyoni mwangu kwa Muislamu yoyote, wala sina husuda moyoni mwangu kwa fadhila yoyote ambayo Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala) amempa mtu yoyote.”
Aliposikia haya, Abdullah bin Amr (radhiya allaahu anhuma) alisema: “Hiki ndicho kitendo ambayo imekufanya wewe kufikia daraja hii ya juu uliyoipata, na hii ndiyo hatua ambayo sisi (watu) hatuwezi kuitekeleza katika maisha yetu.” (Musnad Ahmad #12697, Tareekh Dimashq 20/327, Musnadul Bazzaar #5836)