Uislamu Unakaribisha Nini?

Katika zama za Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam), watu mbalimbali walianza kusilimu.

Ujumbe wa Uislamu ulipoenea na kufikia maeneo mbalimbali, Aksam bin Saifi (rahimahullah), kiongozi wa ukoo wa Tameem, alipendezwa na kujua kuhusu Uislamu. Kwa hiyo, aliwatuma watu wawili kutoka katika kabila lake kusafiri kwenda Madinah Munawwarah ili kufanya utafiti kuhusu Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam) na dini yake.

Watu hawa wawili walipokutana na Rasulullah (sallallahu ‘alaihi wasallam), walieleza kwake kwamba walikuwa wametumwa na kiongozi wao. Kisha wakamuliza Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam), “Wewe ni nani na ujumbe wako ni upi?”

Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) akajibu, “Mimi ni Muhammad, mtoto wa Abdullah, na ninakukaribisha kwenye Uislamu.” Baada ya hapo, Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam) akasoma aya ifuatayo ya Qur’an Majeed:

 إِنَّ اللَّهَ يَأْمُرُ بِالْعَدْلِ وَالْإِحْسَانِ وَإِيتَاءِ ذِي الْقُرْبَىٰ وَيَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ وَالْبَغْيِ ۚ يَعِظُكُمْ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ

Hakika Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala) Anaamrisha kwa uadilifu, wema na kutumia (mali yako) kwa ndugu zako, na anakataza maovu na mabaya. Anakushaurini ili mpate kukumbuka.”

Wale watumwa wawili walipoisikia Aya hii, walivutiwa na ujumbe wake mzito na wa kina, na hivyo wakamuomba Mtume (Sallallahu ‘alaihi wasallam) airudie kwao ili wapate kukariri. Baada ya hapo, walirudi kwa kiongozi wao.

Waliporudi kwa kiongozi wao, walimpa taarifa yote ya mkutano wao. Wakasema: “Tulipouliza kuhusu nasaba yake, alitosha kutaja tu jina lake na jina la baba yake, na wala hakuweka umuhimu wowote kwenye nasaba yake tukufu kama ilivyo kawaida kwa viongozi wa kidunia.

“Lakini, pindi tulipouliza kuhusu nasaba yake kutoka kwa watu, tuligundua kwamba anatoka katika ukoo wa juu sana, safi na adhimu.” Kisha wakasoma Aya ya Qur’an Takatifu mbele yake.

Aksam (rahimahullah) alipoisikia aya hiyo, alisadikishwa juu ya ukweli wa Uislamu na akasema, “Hakika Mtume huyu anaamrisha kwa tabia tukufu na matendo mema, na anakataza tabia za kudharauliwa na vitendo viovu! Wacha tuwe kati ya hao watu wa mwanzo kuishika dini yake, wala tusikawie mpaka tuwe wa mwisho kufanya hivyo.” Baada ya hapo, yeye na kabila lake wakaukubali Uislamu.

Aya Muhimu Na Pana Zaidi Ndani Ya Quran Takatifu

Kwa uhalisia, ujumbe wa ndani uliomo katika aya hii unajumuisha ujumbe mzima na roho ya Uislamu. Inasisitiza umuhimu wa kutimiza haki za Mwenyezi Mungu (subhaanahu wata’aala) na viumbe, pamoja na kuishi maisha ya upendo kamili, usafi, utu na heshima. Hivyo basi, Abdullah bin Mas’ud (radhiyallahu ‘anhu) alitaja kuwa aya hii ndiyo aya pana zaidi ndani ya Quran Majeed.

Kwa ufupi ndani ya aya hii Allah Ta’ala anawaamrisha waumini kusimamisha mambo matatu katika maisha yao na kujiepusha na mambo matatu. Kwa kufanya hivyo, watapata roho ya kweli ya Uislamu.

Mambo matatu tunayoamrishwa kuyashika ni haya:

1. ‘Adl (uadilifu) – kufanya kila kitu na uadilifu kwa kutimiza haki tunazodaiwa na Allah Ta’ala na viumbe.

2. Ihsaan – kupita matakwa ya haki na kuonyesha wema na huruma kwa viumbe.

3. Kuonyesha wema zaidi kwa ndugu zetu, kwa vile Allah Ta’ala amewajaalia kuwa na haki kubwa zaidi juu yetu.

Mambo matatu tunayoamrishwa kujiepusha nayo ni:

1. Mwenendo usio na aibu na tabia mbaya.

2. Dhambi na maovu kwa ujumla.

3. Kudhulumu kwa namna yoyote ile.

About admin

Check Also

Allah Ta’ala – Anaye Ruzuku Viumbe Vyote

Wakati mmoja, kipindi cha Mtume (sallallahu ‘alaihi wasallam), kundi la Maswahabah (radhiyallahu anhum) kutoka kabila …