Tafseer Ya Surah Takaathur

اَلْهٰكُمُ التَّكَاثُرُ ‎﴿١﴾‏ حَتّٰى زُرْتُمُ الْمَقَابِرَ ‎﴿٢﴾‏ كَلَّا سَوْفَ تَعْلَمُوْنَ ‎﴿٣﴾‏ ثُمَّ كَلَّا سَوْفَ تَعْلَمُوْنَ ‎﴿٤﴾‏ كَلَّا لَوْ تَعْلَمُوْنَ عِلْمَ الْيَقِينِ ‎﴿٥﴾‏ لَتَرَوُنَّ ٱلْجَحِيمَ ‎﴿٦﴾‏ ثُمَّ لَتَرَوُنَّهَا عَيْنَ ٱلْيَقِينِ ‎﴿٧﴾‏ ثُمَّ لَتُسْـَٔلُنَّ يَوْمَئِذٍ عَنِ ٱلنَّعِيمِ ‎﴿٨﴾‏

Kushindana baina ya watu katika kukusanya mali (na manufaa ya dunia) kumekushughulisha (kutoka katika utiifu wa Allah Ta‘ala na Akhera). (Hili linaendelea) mpaka mtazuru makaburi (yaani mpaka mtakapofariki). Hapana! hivi karibuni mtakuja kujua (ukweli wa mambo ya dunia ukilinganisha na Akhera, na malengo ya kweli ambayo mlipaswa kuyapigania). Tena, hivi karibuni mtakuja kujua (ukweli). Hapana! Lau mngelijua kwa ujuzi wa yakini (basi msingeghafilika na Akhera). Bila ya shaka mtaliona Moto wa Jahannam. Kisha bila ya shaka mtaliona kwa jicho la yakini. Kisha bila ya shaka mtaulizwa siku hiyo (Siku ya Qiyaamah), kuhusu neema zote (mlizozistarehesha duniani).

اَلْهٰكُمُ التَّكَاثُرُ ‎﴿١﴾‏ حَتّٰى زُرْتُمُ الْمَقَابِرَ ‎﴿٢﴾‏

Kushindana baina ya watu katika kukusanya mali ( na manufaa ya dunia) kumekushughulisha (kutoka katika utiifu wa Allah Ta‘ala na Akhera). (Hili linaendelea) mpaka mtazuru makaburi (yaani mpaka mtakapofariki).

Kushindana baina ya watu katika kukusanya mali na manufaa ya kidunia kumegeuza mazingatio ya mwanadamu kutoka kwenye lengo lake kuu maishani. Makusudio na shabaha kuu ya maisha ya mwanadamu ni kupata radhi za Allah Ta’ala na kujitahidi na kufanya bidii kwa ajili ya Kupata Jannah. Kwa bahati mbaya, kutokana na kupenda sana mali na utambuzi wa kidunia, mwanadamu anakengeushwa kutoka kwenye kusudi lake kuu na anajihusisha katika kushindana na wengine kwa ajili ya manufaa ya kidunia.

Katika Aya hii, Allah Ta’ala anamlalamikia mwanadamu – kwamba anaendelea na mashindano haya hadi mwisho wa maisha yake, mpaka hatimaye akafika kaburini.

Abdullah bin Shikheer (Radhiya Allaahu ‘anhu) anaripoti, “Wakati mmoja nilimtembelea Rasulullah (Sallallaahu ‘alaihi wasallam) alipokuwa akisoma surah hii. Baada ya kusoma surah hii, Rasulullah (Sallallaahu ‘alaihi wasallam) alisema: “Mwana wa Aadam (kwa kujifakhirisha) anasema, ‘Mali yangu, mali yangu.’ Hata hivyo hakuna faida kwenu katika mali zenu isipokuwa ile mliyokula na kuimaliza, au mliyovaa mpaka ikazeeka, au mliyotoa kwa sadaka na mkaitanguliza (Akhera).

Katika riwaya ya Muslim, Rasulullah (Sallallaahu ‘alaihi wasallam) pia ametaja kwamba kila mali, mbali na hizi zilizotajwa katika Hadith hapo juu, zitaachwa kwa ajili ya watu wengine (yaani warithi wake).

Ni asili na mwelekeo wa mwanadamu kwamba hato ridhika na mali aliyonayo na kwa hiyo anaendelea kujituma kukusanya mali na kuziongeza. Kuhusiana na tamaa isiyotosheka ya mwanadamu na kutafuta mali, Rasulullah (Sallallaahu ‘alaihi wasallam) amesema, “Ikiwa mwana wa Aadam ana bonde la dhahabu, atatamani bonde la pili la dhahabu. Na hakuna kitakachojaza tumbo la mwanadamu isipokuwa mchanga wa kaburi. Na Allah Ta’ala atapokea toba ya mwenye kutubia kwake.” (Sahih Bukhaari #6436)

‏كَلَّا لَوْ تَعْلَمُوْنَ عِلْمَ الْيَقِينِ ‎﴿٥﴾‏

Hapana! Lau mngelijua kwa ujuzi wa yakini (basi msingeghafilika na Akhera)

Katika Aya hii, Allah Ta’ala Anasema: “Lau mngelijua kwa ujuzi wa yakini (basi msingeghafilika na Akhera).”

Kwa maneno mengine, lau ungetafakari juu ya ukweli wa kifo na kutafakari juu ya mwisho wako, wakati utakapokuwa umelala kaburini ukiwa peke yako, na fahari na utukufu uliyokuwa ukifurahia sasa umetoweka, basi usingeghafilika na faradhi zako kwa Allah Taala na pia usingeghafilika na Akhera.

لَتَرَوُنَّ ٱلْجَحِيمَ ‎﴿٦﴾‏ ثُمَّ لَتَرَوُنَّهَا عَيْنَ ٱلْيَقِينِ ‎﴿٧﴾

Bila ya shaka mutauona Moto wa Jahannam. Kisha bila shaka mutauona kwa jicho la yakini.

Kuna viwango viwili vya uhakika. Kiwango cha kwanza ni elimu ya yakini ambayo mtu anayo katika akili yake, na kiwango cha pili ni elimu inayopatikana kupitia jicho la yakini, ambapo mtu huona ukweli mbele ya macho yake mwenyewe.

Kwa hakika, kuona uhalisi wa jambo fulani hujenga kiwango tofauti cha yakini ikilinganishwa na kuwa na elimu wa jambo hilo tu.

Kwa mfano, mtu ana elimu wa nyoka na madhara ambayo inaweza kusababisha. Lakini, anapokutana uso kwa uso na nyoka na kukutana na madhara zake, basi uhakika wake na usadikisho wa nyoka na madhara yake hufikia kiwango tofauti.

Moosa (‘alaihis salaam) alijua kuhusu qudra ya Allah Ta’ala na alijua kuhusu nyoka. Lakini, pale Allah Ta‘ala alipomuamuru kuitupa fimbo yake na ikabadilika na kuwa nyoka, hapo hapo aligeuka na kuanza kukimbia. Kwa hivyo, kuona uhakika wa kitu ni tofauti na kuwa na elimu tuu na kitu fulani.

‏ ثُمَّ لَتُسْـَٔلُنَّ يَوْمَئِذٍ عَنِ ٱلنَّعِيمِ ‎﴿٨﴾‏

Kisha bila ya shaka mtaulizwa siku hiyo (Siku ya Qiyaamah), kuhusu neema zote (mlizozistarehesha duniani).

Siku ya Qiyaamah, mtu ataulizwa kuhusu neema zote alizozipata hapa duniani. Ataulizwa kuhusiana na afya yake, mali yake, muda wake n.k. Katika Aya nyingine ya Qur-aan Takatifu, Allah Ta’ala Anasema:

اِنَّ ألسَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُوْلَٰٓئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْـٔولًا

Hakika sikio, jicho na moyo (yaani akili) – yote haya (neema) mtaulizwa na kutolewa hisabu (Siku ya Qiyaamah).

Kutokana na Aayah hii, tunaelewa kwamba Siku ya Qiyaamah, mtu ataulizwa kuhusu uwezo wa kusikia, kuona na kuelewa n.k mtu ataulizwa kama mtu alitumia uwezo huu kujishughulisha na dhambi au alizitumia katika kumuabudu Allah Ta’ala. Vile vile mtu ataulizwa kuhusiana na nia aliyokuwa nayo wakati wa kutekeleza amali njema na fikra alizokuwa nazo akilini mwake kuhusu Allah Ta‘ala au viumbe.

Katika Hadith moja, Rasulullah (Sallallaahu ‘alaihi wasallam) ametaja kuwa Siku ya Qiyaamah, mtu atakapodhihiri kwenye tambarare za Qiyaamah, hatoweza kutoka mahala pake mpaka ajibu maswali matano. Maswali haya matano yatahusu neema tano maalum za Allah Ta’ala alizozifurahia duniani:

1) Alipataje utajiri wake?

2) Alitumiaje mali yake?

3) Alitumiaje ujana wake?

4) Alitumiaje maisha yake?

5) Je! ni kiasi gani alichofanya juu ya elimu ya dini aliyojifunza?

Kwa ujumla, watu huona ujuzi kuwa kitu cha kujivunia. Lakini, ikumbukwe kwamba elimu ya Dini ni neema kubwa ya Allah Ta’ala juu ya mtu, kiasi ataulizwa Siku ya Qiyaamah.

Siku ya Qiyaamah, kila mtu ataulizwa ni kiasi gani alichofanya juu ya elimu ya Dini aliyoipata. Kwa hivyo, kama alipata elimu ya Dini lakini hakuifanyia kazi, atashughulikiwa kwa kutoitumia elimu ya Dini.

About admin

Check Also

Tafseer Ya Surah Lahab

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ تَبَّتْ يَدَا أَبِي لَهَبٍ وَتَبَّ ‎﴿١﴾‏ مَا أَغْنَىٰ عَنْهُ مَالُهُ وَمَا كَسَبَ ‎﴿٢﴾‏ سَيَصْلَىٰ نَارًا …