وَالتِّينِ وَالزَّيْتُونِ ﴿١﴾ وَطُورِ سِينِينَ ﴿٢﴾ وَهَـٰذَا الْبَلَدِ الْأَمِينِ ﴿٣﴾ لَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ فِي أَحْسَنِ تَقْوِيمٍ ﴿٤﴾ ثُمَّ رَدَدْنَاهُ أَسْفَلَ سَافِلِينَ ﴿٥﴾ إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ فَلَهُمْ أَجْرٌ غَيْرُ مَمْنُونٍ ﴿٦﴾ فَمَا يُكَذِّبُكَ بَعْدُ بِالدِّينِ ﴿٧﴾ أَلَيْسَ اللّٰـهُ بِاَحْكَمِ الْحَاكِمِينَ ﴿٨﴾
Na aapa kwa mtini na mzeituni; na kwa Mlima wa Toori wa Seeneen- Mlima Sinai; na kwa mji huu wa amani. Hakika Sisi tumemuumba Mwanaadamu kwa muundo bora zaidi kabisa. Kisha tutamrudisha chini kuliko walio chini. Isipokuwa wale walio amini na wakatenda mema; kwao watapata malipo yasiyoisha. Basi nini kitakufanyeni baada ya hayo yote ukanushe malipo? Je! Allah Ta’ala si Hakimu muadilifu kuliko mahakimu wote.?
وَالتِّينِ وَالزَّيْتُونِ ﴿١﴾ وَطُورِ سِينِينَ ﴿٢﴾وَهَـٰذَا الْبَلَدِ الْأَمِينِ
Na aapa kwa mtini na mzeituni; na kwa Mlima wa Toori wa Seeneen- Mlima Sinai; na kwa mji huu wa amani.
Katika Aya hizi tatu, Allah Ta’ala anakula viapo vinne kwenye sehemu tukufu za dunia. Maeneo haya ni sehemu za baraka kubwa na wakati fulani palikuwa ni vituo vya mwongozo kwa Ambiyaa mbalimbali (‘alaihimus salaam).
“Mtini na mzeituni” zilizotajwa katika Aya ya kwanza zinahusu ardhi zilizobarikiwa za Palestina na Shamu, sehemu ambazo matunda haya yanapandwa kwa wingi na ambapo wengi wa Ambiyaa (‘alaihimus salaam) walihubiri dini ya Allah Ta‘ala. Palestina, hasa, palikuwa mahali alipozaliwa Nabi Isa (‘alayhis salaam) na kitovu alichohubiri mwongozo.
Tur, mlima wa Sinaai, ni mlima ambao juu yake Taurati ilitolewa kwa Nabi Musa (‘alayhis salaam).
“Mji huu wa amani” unamaanisha mji mtakatifu wa Makkah Mukarramah, ambamo kuua mtu au mnyama yoyote ni marufuku. Mji mtukufu na wa amani wa Makka Mukarramah ni mji mkubwa na uliobarikiwa zaidi kutoka katika miji yote duniani, na ni mahali pa kuzaliwa na nyumbani kwa Mtume wa mwisho wa Allah Ta’ala, Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam) kabla yake kuhama kuelekea Madina Munawwarah.
Kwa hivyo, katika aya hizi, Allah Ta’ala anakula kiapo juu ya ardhi hizi zilizobarikiwa kwa sababu ya neema nyingi zinazopatikana humo.
لَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ فِي أَحْسَنِ تَقْوِيمٍ ﴿٤﴾ ثُمَّ رَدَدْنَاهُ أَسْفَلَ سَافِلِينَ ﴿٥﴾ إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ فَلَهُمْ أَجْرٌ غَيْرُ مَمْنُونٍ ﴿٦﴾ فَمَا يُكَذِّبُكَ بَعْدُ بِالدِّينِ ﴿٧﴾ أَلَيْسَ اللّٰـهُ بِاَحْكَمِ الْحَاكِمِينَ ﴿٨﴾
Hakika sisi tumemuumba mwanadamu kwa muundo bora zaidi kabisa. Kisha tutamrudisha chini kuliko walio chini. Isipokuwa wale walioaamini na wakatenda mema; kwao watapata malipo yasioisha. Basi nini kitakufanyeni baada ya hayo yote ukanushe siku ya Qiyaamah? Je! Allah Ta’ala si hakimu muadilifu kuliko mahakimo wote?
Baada ya kula viapo vinne juu ya ardhi hizi zilizobarikiwa, Allah Ta‘ala anataja ujumbe unaoelekezwa kwa mwanadamu kupitia viapo vinavyochukuliwa. Allah Ta’ala Anasema, “Hakika Sisi tumemuumba Mwanaadamu kwa muundo bora zaidi”. Kwa maneno mengine, mwanadamu anapaswa kutafakari juu ya ukweli kwamba kama vile Allah Ta’ala amezichagua ardhi hizi kuwa ardhi kubwa na yenye baraka tele duniani, vivyo hivyo Allah Ta’ala amemchagua mwanadamu kuwa kiumbe chake bora zaidi duniani na alimuumba katika utunzi bora.
Ikiwa mwanadamu atarekebisha maisha yake na akafuata mwongozo ulioteremshwa na Allah Ta’ala kwa Rasulullah (Sallallahu ‘alaihi wasallam), basi ataweza hata kuwapita Malaika kwa daraja. Kwa hivyo, ikiwa atajidhalilisha kwa kuishi maisha ya dhambi na maovu, basi atashushwa chini kabisa mbele ya Allah Ta‘ala.
Baadhi ya wafasiri wanaeleza kwamba “mtungo bora zaidi” uliotajwa katika Aayah unarejelea kwenye muundo wa kimaumbile na uwezo wa mwanadamu ambao uko kwenye kilele chake wakati wa awali ya maisha yake. Kwa hivyo, mara tu anapokaribia uzee, huanza kupoteza uzuri wake wa nje na nguvu za kimwili, mpaka kufikia hatua ya chini ya udhaifu. Kwa hivyo, katika Aya hii, Allah Ta‘ala anataja kwamba ingawa hali yake ya kimwili inazidi kuzorota na kudhoofika, bado anaheshimiwa na Allah Ta‘ala, na matendo mema aliyoyafanya yataendelea kuongezeka Akhera.
فَمَا يُكَذِّبُكَ بَعْدُ بِالدِّينِ ﴿٧﴾ أَلَيْسَ اللّٰـهُ بِاَحْكَمِ الْحَاكِمِينَ ﴿٨﴾
Basi nini kitakufanyeni baada ya hayo yote ukanushe malipo? Je! Allah Ta’ala si hakimu muadilifu kuliko mahakimo wote?
Katika aya zilizotangulia, Allah Ta‘ala anamkumbusha mwanadamu kwamba Allah Ta‘ala amemuumba katika utungo bora kabisa na amemfanya kuwa wa kipekee kutoka katika viumbe vingine vyote. Hata hivyo, Allah Ta’ala pia anamfahamisha kwamba maendeleo yake na mafanikio yake yanategemea juu yake kuishi maisha ya uchamungu na uadilifu. Ikiwa ataishi maisha ya dhambi, atadhalilishwa mpaka chini kabisa na atapoteza heshima yake mbele ya Allah Ta’ala. Vile vile, anafahamishwa kwamba baada ya kufurahia muda wa nguvu, nguvu zake zitapungua polepole na kufikia uzee. Kwa hiyo, anapaswa kuchukua somo kutokana na hili na kutambua kwamba baada ya maisha haya, kuna maisha mengine yajayo yaani maisha ya milele ya Akhera.
Katika aya hii, Allah Ta‘ala anamfahamisha mwanadamu kuhusu mwisho wake, kwamba hatimaye atafika kaburini na italazimika asimame mbele ya Allah Ta‘ala Siku ya Qiyaamah. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala): “Ni nini kitakachokufanyeni baada ya haya yote ukanushe Siku ya Qiyaamah? Kwa maneno mengine, pale mwanadamu alipoyaona mabadiliko katika maisha yake na akatambua kwamba siku moja atakufa, basi inakuwaje anakataa maisha ya Akhera?